Wanakijiji wenzangu,KWA heshima kubwa kwenu nawatumia salamu za Heri na Fanaka ya Mwaka Mpya wa 2009 nikiwa nimesimama pwani ya Bagamoyo kwenye bahari ya Hindi.
Ndugu Wanakijiji wenzangu, nina furaha kuwajulisha kuwa k mwaka huu tunaoumaliza, kijiji chetu kimeendelea kupata mafanikio ya kuridhisha.
Kama ilivyokuwa kwa mwaka jana, Kijiji kimekuwa chachu ya mijadala yenye kulenga kwenye kulinda maslahi mapana ya nchi yetu. Kijiji chetu kimetembelewa na watu wengi. Takwimu zinaonyesha watembeleaji zaidi ya 12,000 ( wenye IP address) wameingia kijijini. Kuna ‘hits’ takribani laki saba zenye wastani wa ‘ hits’ 2500 katika saa 24. Haya ni mafanikio yanayotokana zaidi na juhudi zenu za kuchangia maoni na hivyo kufanya mahali hapa kuwa pa kuwavutia watu kuja kutembelea. Nawahakikishia kuwa maoni yanayochangiwa humu yanasomwa na watu wa kada zote ikiwamo na tuliowapa dhamana za uongozi.
Hakika mijadala mingi humu kijijini imekuwa yenye siha. Kwa baadhi yetu imekuwa ni darasa tosha la kujichotea maarifa mbalimbali. Na tuendelee kukifanya kijiji hiki kuwa chachu ya mijadala hata mwaka ujao wa 2009.
Ni dhahiri kuwa wakati mwingine kumekuwa na joto kali la mijadala. Kuna waliokwazwa katika hilo. Na tuamini kuwa wengi wameshiriki mijadala wakiwa na dhamira njema.
Mwisho, kazi tuifanyao humu ni ya kibinadamu na ya hiyari. Mapungufu hayakosekani. Tushirikiane katika kukosoana kwa lengo la kujenga.
Nawatakia mwisho mkamilifu na HERI YA MWAKA MPYA!
Pamoja Tuijenge Nchi Yetu
Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania.
Ahsanteni,
Maggid
Bagamoyo, Desemba 31, 2008.


















































Tanzanian Shilling Converter