


TAHARIRI: HUU NDIO MSIMAMO WETU
NDUGU Msomaji, leo Jumanne Machi 31, 2009 , Tanzania kama nchi imeendelea kufurahia uhuru wa kutoa maoni kwa njia ya vyombo vya habari. Hii ni kwa kuwa na gazeti jipya na huru la ‘Kwanza Jamii’. Hivyo basi, unalolisoma sasa kwa mara ya kwanza ni gazeti la ‘ Kwanza Jamii’. Kama ilivyo kwa jina lake, ni gazeti la jamii, ni gazeti lako.
Kwanza Jamii ni gazeti la kijamii lililoanzishwa na wanajamii kwa ajili ya wanajamii wa Kitanzania ndani na nje ya mipaka yetu. Pamoja na nia ya kibiashara kwa maana ya kupata faida, waanzilishi wa gazeti hili wamesukumwa na vipaumbele vikuu viwili; mosi, tunaamini kwamba nchi hii imejaaliwa kuwa na vyombo vingi vya habari vinavyojumuisha redio , magazeti na televisheni.
Na tunaamini pasi na shaka, kuwa kuna Watanzania wengi hawapajapata nafasi ya kutosha kutoa maoni yao kwa nia ya kushauri, kukosoa, na hata kupongeza juu ya mustakabali wa mwenendo mzima wa utendaji wa vyombo mbalimbali vya usimamizi wa rasilimali za umma na usimamizi wa mifumo mbalimbali ya kiutawala.
Hivyo basi, Kwanza Jamii tuna azma ya kupanua wigo kwa Watanzania kupata nafasi hiyo ya kupata habari, kuelimika na kuburudika . Si hivyo tu, na hata Watanzania wenyewe, kupitia kalamu zao, kompyuta na simu zao, kusema yale wanayotaka kusema kupitia gazeti hili. Maana, Kwanza Jamii ni gazeti lao bila kujali tofauti za kikabila, kidini na kirangi.
Pili, zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanaishi vijijini. Kwanza Jamii litashirikiana kwa karibu na ndugu zetu hao ili kubaini kero, karaha, taabu na hata raha wanazozipata kwenye maeneo yao hayo. Ingawa jambo hilo lina gharama, lakini tunaahidi kujitahidi kuwafikia Watanzania wenzetu hawa kwa namna moja au nyingine.
Tunajua , kuwa wapo wenzetu mahodari wa kusema bayana kwa nia njema, lakini pia, miongoni mwa asilimia 80 hiyo ya Watanzania, wapo wasioridhishwa na mambo fulani fulani kwenye mfumo wetu wa kimaisha. Hata hivyo, kwa sababu mbalimbali, hawana uwezo wa kunyanyua kalamu au ndimi zao na kukemea. Hawa tunawaomba wasifadhaike na kukata tamaa.
Kwanza Jamii tumejipanga na tumewaletea wachambuzi wanazuoni na wasio wanazuoni. Ni wachambuzi mahiri kabisa katika maeneo yao. Na tuamini, kuwa wapo tayari kuwaondoa upweke na kusemea mioyo yenu kwa nia njema kabisa ya kushiriki kuijenga nchi yetu. Maana, hawa ni wasomi waliosomeshwa kwa kodi za wanajamii walio wengi wa kule vijijini. Ni jukumu la wasomi hawa kuanza kutumia maarifa yao kuisaidia jamii pana walioiacha nyuma yao.
Na katika zama hizi za kuwafichua wabadhilifu wa mali za umma waliojipatia jina jipya la mafisadi, inasemwa mitaani, kuwa mafisadi hao wameanzisha, na wanaendelea kuanzisha na hata kuvifadhili vyombo vya habari na wanahabari wenyewe kwa nia ya kufunika maovu yao. Sisi- Kwanza Jamii, tunaomba tujipambanue kungali mapema, kuwa gazeti hili halikuanzishwa kwa faida iliyotokana na shughuli zozote za kifisadi.
Hivyo basi, tunatoa wito kwa wale wote wanaojijua, kuwa wanachuma mali zao kwa njia za kifisadi, kuwa gazeti hili si mahali salama pa kukimbilia ili kuwapakizia ubaya wale waliobaini unyang’au wao. Kwanza Jamii tunaahidi pia kushirikiana na wale wote wanaokandamizwa kutokana na mfumo wa uongozi kwenye vijiji vyao, mitaa yao, makazini na hata majumbani mwao. Ingawa , katika kufanya hivyo, hatuko tayari kuingilia uhuru wa familia bila utashi wa wahusika. Kwamba tutazingatia miiko ya taaluma ya uandishi wa habari. Na tukumbuke, hakuna uhuru usio na mipaka.
Kwanza Jamii tutapigana bega kwa bega na wale wote walio tayari na wenye dhamira ya dhati ya kupambana na maovu katika jamii yetu. Kwanza Jamii tutakosoa kwenye makosa na tutashauri penye mkanganyiko. Lakini pia hatutasita kusifu na kupongeza panapostahiki.
Kwanza Jamii hatutamwonea mtu au taasisi yeyote ile kwa dhamira na makusudi ya kutaka kuonea. Na katu hatutomwogopa wala kumwonea aibu yeyote atakayekiuka utaratibu wa kisheria tuliojiwekea katika mfumo wa maisha yetu, uongozi wetu, siasa zetu na tamaduni zetu .
HUU NDIO MSIMAMO WETU.




Tanzanian Shilling Converter
7 comments:
Mkuu,
Gazeti lina-share siku ya moja ya kuzaliwa nami.
Hongereni kwa kazi kubwa na nzito ya kutoa toleo la kwanza.
Changamoto kubwa tuliyonayo kwa uandishi wa habari wa Tanzania ni kuwa na habari zilizosimama kwenye ukweli bila kupindisha, zenye kina na uchambuzi wa kutosha.
Natumai gazeti lenu litazingatia haya.
Mimi na nyie tunahitaji pongezi siku ya leo. Hongereni!
Mdau
Faustine
http://drfaustine.blogspot.com/
Mwenyeketi mbona wasiwasi, kwa nini useme kuwa "bila kujali ukabila" labda 'ukabila' lakini kwa udini mwenzangu hapana, 'udini' hupo tena mkubwa, soma articles zako vizuri hasa zile za Israel etc, mwenyekiti haya kazi njema, tunangojea gazeti hilo, sisi ni wasomaji bwana,
Mzee, nina article yangu nitakutumia uweze kupost- Big-up, huo ndio ujasiliamali
Mwana kijiji Unabahati kwani sasa serikali inampango wa kubinafsisha magazeti yote kwa wawekezaji wa kigeni.
hakuna hata wavuti au tovuti ya gazeti...
MJENGWA SIO MDINI AMEJAZA WAKRISTU WATUPU KWENYE GAZETI HILI.WADINI KAMA MWANAKIJIJI NA JAMBOFORUMS MADA ZAO KUKASHFU OIC,MAHAKAMA YA KADHI N.K
HONGERA MAJJID UNA DIZEVU HAYA UMETOKA MBALI SANA.
SURA YA KWANZA INAYOONEKANA KWENYE GAZETI LENU INAONESHA WAZI MSIMAMO WENU KUWA MTAJIKITA SANA KWENYE HABARI ZA VIONGOZI NA SI ZA WANANCHI. MMEANZIA NA KARUME MTAENDEOLEA HIVYOHIVYO KWANI MNAHISI KUWA HIZO NDIYO HABARI.
Post a Comment