We have 234 guests and no members online

Afrika mmemsikia Mugabe?

Posted On Monday, 24 February 2014 08:29 Written by
Rate this item
(0 votes)

mugabe_8316d.jpg

Na Fadhy Mtanga

WAKATI Afrika inatingwa na pilika za wanasiasa wa kisasa wanaojali posho na madaraka, kiasi cha kuzisahau harakati za Waafrika wazalendo walioifanya Afrika kuwa huru, huko Kusini mwa Afrika, kwenye nchi masikini ya Zimbabwe, Mwafrika Robert Mugabe anapiga mbiu. Anaipaza sauti yake iliyochoka kutokana na umri wa miaka 90 anaousherehekea sasa. Miaka 90 hiyo pengine imetosha kumwondolea kumbukumbu ya mambo yaliyotukia zaidi ya miaka 50 sasa humu barani Afrika. Lakini, umri huo haumfanyi Robert Mugabe kumsahau jemedari wa ukombozi wa Kusini mwa Afrika, Afrika yote na ulimwenguni kwa ujumla wake, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Pamoja na kuwa komredi Bob Mugabe anashindwa kuwa mwanafunzi mweledi wa Mwalimu Nyerere, kwa kung'ang'ania kubaki madarakani kwa miaka 35 sasa toka taifa lake lipate uhuru, hawi mnafiki kwa kushindwa kumsemea yalo mema Mwalimu Nyerere. Mugabe, ameshindwa kuishi kwa mfano wa mpigania uhuru huyo. Mwalimu aliondoka madarakani kwa hiyari yake mwenyewe huku akiitajirisha lugha adhimu ya Kiswahili kwa kuongeza msamiati 'kung'atuka' alioutoa huko kwao Uzanaki.

 

Ikiwa ni miaka 15 sasa toka kufariki kwa Mwalimu Nyerere, Robert Mugabe anasherehekea miaka 90 ya kuzaliwa kwake. Sherehe inafana kweli kweli. Rais mkongwe zaidi anakisogelea kipaza sauti. Pasipo kumung'unya maneno, anasema, "Huu ni wakati wa Afrika kumheshimu mkombozi Nyerere."

Robert Gabriel Mugabe anaongea mengi. Anasema, "Ninataka kusema, wakati heshima zimekuwa zikimwagwa kwa mashujaa wa Afrika, mtu anayenyanyaswa ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Hapa tulipo, mapambano ya ukombozi, tulitegemea rasilimali kutoka Tanzania. Lakini hakuna kinachosemwa kuhusu huyu mtu na nchi yake katika OAU. Nkurumah, ndiyo, alikuwa na msaada...Lakini Tanzania, kusema Nyerere alikuwa kama wengine tunakosea.

Mugabe akawaambia Wazimbabwe, "Ninataka sisi, Wazimbabwe, kusimama upande wa Nyerere. Afrika inapaswa kukumbushwa juu ya wajibu uliosukumwa kwa mtu huyu, mzigo wa kuwafunza wapigania uhuru wote. Mzigo huu si wa kisiasa tu, lakini, mwishowe, hakuna mtu anayesema Tanzania inastahili kutajwa."

Mugabe hakupungukiwa maneno juu ya Mwalimu Nyerere na Tanzania. Akaendelea, "Wote tulikwenda njia tofauti, katika miktadha tofauti, kwa Tanzania kuzikomboa nchi zetu, sote hatujarudi Tanzania. Sawa, nitakuwa mwenyekiti wa AU hivi karibuni na ninakwenda kulishughulikia hili jambo. Hakuna, hakuna, hakuna, hakuna anyethamini alichokifanya Nyerere."

Afrika mmemsikia Mugabe? Hivi ndivyo alivyoweza kuzungumza juu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyezaliwa kijijini Butiama mkoani Mara mwaka 1922. Baada ya miaka 77 ya kuishi kwake, Mwalimu Nyerere akaaga dunia mwaka 1999 akiwa kwenye matibabu huko London, nchini Uingereza.

Pamoja na kuisaidia nchi yake ya Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961, Mwalimu Nyerere atakumbukwa kwa falsafa yake ya kuona uhuru wa Tanganyika si lolote ilhali Waafrika wengine wakiwa wangali wamefungwa na minyororo mizito ya ukoloni. Akazisaidia nchi za Kusini mwa Afrika kwa mafunzo na vifaa ili zipate uhuru. Hayo hayakutosha. Akapaza sauti yake kwa ajili ya wanadamu wengine wanaokandamizwa kote ulimwenguni.

Je, Afrika haiyakumbuki yote hayo kiasi cha kudiriki hata kuiondoa picha yake kwenye bango la waasisi wa Muungano wa Afrika lililopo jijini Addis Ababa? Katika kipindi cha miaka 50 tu imetosha kusahau mchango wake?

Afrika imetingwa na kutawaliwa na viongozi wapenda madaraka na posho.

Read 1218 times

Add comment


Security code
Refresh

Tafuta Habari

Blog Shabihana

Maji